(ABNA24.com) Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran na Islamabad zinaamini kuwa, masuala ya kieneo yanapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo baina ya nchi mbalimbali.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan na kuongeza kuwa: Katika mazungumzo yao pande hizo mbili zimetilia mkazo umuhimu wa amani ya eneo nyeti la Ghuba ya Uajemi na kwamba, ufunguo wa utatuzi wa masuala ya eneo hilo ni kukomeshwa vita vya Yemen na kusitisha mapigano mara moja.
Rais Rouhani pia ameashiria vikwazo vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na kusema: Katika mazungumzo haya pande mbili zimevitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Iran kuwa ni ugaidi wa kiuchumi na kutangaza kuwa, Marekani inapaswa kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kufuta vikwazo hivyo ili kuweza kutatua kadhia hiyo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema kuwa lengo la safari yake mjini Tehran ni kuzuia mapigano na mvutano mpya katika Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa: Pakistan imepata mashaka makubwa katika kipindi cha miaka 15 kutokana na mapigano na imepoteza watu elfu 70 katika vita dhidi ya ugaidi.
Waziri Mkuu wa Pakistan pia ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa himaya na uungaji mkono wake kwa watu wa Kashmir.
Waziri Mkuu wa Pakistan amewasili mjini Tehran leo kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran.
/129
14 Oktoba 2019 - 06:58
Msimbo wa Habari: 982505
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran na Islamabad zinaamini kuwa, masuala ya kieneo yanapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo baina ya nchi mbalimbali.